Disable Preloader

News

MATEMBEZI JUMUISHI YA HISANI YA MAADHIMISHO YA WIKI YA KIMATAIFA YA WATU WENYE ULEMAVU DUNIANI, TAREHE 29 NOVEMBA 2020.

Taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa na bi. Shimimana ntuyabaliwe, mkurugenzi wa taasisi ya dr. Reginald mengi persons with disabilities foundation (drmf) tarehe 13 oktoba 2020

Kuhusu matembezi jumuishi ya hisani ya maadhimisho ya wiki ya kimataifa ya watu wenye ulemavu duniani, tarehe 29 novemba 2020.

Ndugu wanahabari, Kwa niaba ya bodi ya wadhamini ya Dr. Reginald Mengi Persons with Disabilities Foundation, nachukua fursa hii kwa heshima na taadhima kuwakaribisha kwenye ofisi zetu za foundation.

Ndugu wanahabari, kama mnavyofahamu muasisi wetu marehemu Dr. Reginald Mengi, alijitoa sana kwa hali na mali katika kujenga utu na ustawi wa watu wenye ulemavu hapa Tanzania. Kazi hii aliifanya kwa zaidi ya miongo mitatu. Hivyo basi taasisi hii ambayo aliizindua mwaka 2018, imebeba pamoja na mambo mengine jukumu kubwa la kulinda na kuenzi legacy yake kwa kuendeleza kazi hii ya kuwahudumia watu wenye ulemavu.

Ndugu wanahabari, kwa niaba ya bodi ya wadhamani wa taasisi yetu, napenda kuwafahamisha umma wa watanzania kuwa leo tuzindua rasmi kampeni ya maadhimisho ya mtu mwenye ulemavu duniani kwa mwaka 2020, kupitia matembezi jumuishi ya hisani

Ndugu wanahabari, matembezi haya jumuishi ya hisani yamebeba kauli mbiu ya Umoja wa Mataifa ya siku ya mtu mwenye ulemavu duniani ya mwaka huu 2020, inayosema “Sio Kila Ulemavu Unaonekana” (Not All Disabilities are visible). Matembezi haya jumuishi yameandaliwa yakiwa na njia tatu ili kuruhusu watu wenye ulemavu na wasio na ulemavu kushiriki. Hususani, kutakuwa na ushiriki wa kilomita mbili na nusu, tano pamoja na kumi.

Ndugu wanahabari, Matembezi haya yanatarajiwa kufanyika katika viwanja vya Mnazi Mmoja, jijini Dar es Salaam na Mgeni Rasmi anatarajiwa kuwa Mheshimiwa Mama Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Raisi wa Jamuhuri ya Muungano ya Tanzania.

Ndugu wanahabari, Lengo la matembezi haya ni kuelimisha na kuhamasisha jamii ili waweze kutambua aina mbalimbali za ulemavu hususani ule ambao hautambuliki kwa urahisi.

Ndugu wanahabari, Katika matembezi haya taasisi yetu imechagua Ulemavu wa Akili, Ulemavu wa Kisaikolojia na Usonji ili jamii pamoja na wadau mbalimbali waweze kuutambua ulemavu huu, kufahamu changamoto mbalimbali zinazohusu aina hizi za ulemavu na kushirikiana kwa pamoja katika kutoa huduma zinazo hitajika kwa watu wenye ulemavu huu.

Ndugu wanahabari, Shirika la Afya duniani linakadiria kuwa ifikapo mwaka 2030, ulemavu wa akili na kisaikolojia utakua sana na kuwa na idadi kubwa ya wahanga kupita aina nyingine za ulemavu. Hii itasababisha gharama za matibabu pamoja na gharama za kiuchumi kwa dunia kuwa kubwa na kuleta changamoto kwa jamii. Hivyo basi matembezi haya yamelenga kuibua vipaumbele kwa wadau mbalimbali nchini ili tuweze kujipanga na kukabiliana na changamoto hii sasa na kwa siku za usoni.

Ndugu wanahabari, fedha zitakazopatikana kutokana na kampeni hii zitatumika;

 • Kuchangia gharama za dawa za kila mwezi za wagonjwa wa afya ya akili. Dawa hizi ni ghali lakini ni muhimu sana katika kulinda na kujenga afya ya akili.
 • Pili kwa kushirikiana na wataalamu wa afya ya akili wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, tutaendesha kambi mkoba za afya ili kutoa elimu pamoja na huduma ya uchunguzi kwa walengwa ikiwa ni pamoja na kwa watoto wenye usonji. Kambi hizi zitafanyika katika mikoa ambayo ina matukio mengi ya watu wenye ulemavu wa akili, ulemavu wa kisaikolojia pamoja na usonji, (Dar es Salaam, Kilimanjaro, Iringa na Singida).

Ndugu wanahabari, ili kufanikisha matembezi haya taasisi yetu inashirikiana na wadau mbalimbali ili kuhakikisha kuwa matembezi haya ni jumuishi. Wadau hawa ni kutoka katika vyama vya watu wenye ulemavu, vyama vya madaktari na wataalamu wa afya ya akili, wazazi wenye watoto wenye usonji pamoja na ulemavu wa akili na taasisi zinazotoa huduma kwa makundi haya. Wadau hawa ambao baadhi yao wamewakilishwa hapa ni pamoja na;

 • Mental Health Association of Tanzania (MEHATA)
 • Tanzania Users and Survivors of Psychiatric Organization (TUSPO)
 • Tanzania Association of Mentally Handicapped (TAMH)
 • Unique Child Academy Iringa
 • Tanzania Autism Resource Centre
 • Tanzania National Association for People with Autism (NAPA-T)
  • Ndugu wanahabari, basi nichukue fursa hii kuwaalika ndugu zetu watanzania, taasisi, mashirika pamoja na vyombo vya habari kutuunga mkono na kujitolea kwa hali na mali ili makundi haya yaweze kupata msaada ambao wanauhitaji sana.

   Ndugu wanahabari, tuna njia mbalimbali za ushiriki wa mtu mmoja mmoja ikiwa ni pamoja na kupitia kwenye tovuti yetu ya www.drmengifoundation.org; akaunti zetu za mitandao ya kijamii za facebook, twitter na instagram @drmengifoundation pamoja na vituo vya kujiandikisha kushiriki vitakavyotangazwa kupitia vyombo vya habari hapo baadae.

   Ndugu wanahabari, tunakaribisha makampuni mbalimbali kushiriki kupitia udhamini wa matembezi haya ikiwa ni pamoja na kudhamini ushiriki wa watu wenye ulemavu. Tuna viwango mbalimbali vya udhamini wa matembezi haya ambavyo vinapatikana katika tovuti yetu pamoja na vipeperushi.

   Ndugu wanahabari, Kwa niaba ya bodi ya wadhamini wa taasisi yetu ya Dr. Reginald Mengi, PWD Foundation, nichukue fursa hii kuwashukuru sana vyombo vyote vya habari pamoja na wanahabari kwa ushirikiano mkubwa mnaoipa taasisi yetu. Vilevile nawashukuru sana kwa nzuri mnayoifanya ya kuelimisha jamii kuhusu changamoto za watu wenye ulemavu, mafanikio na nafasi yao katika jamii.

   ASANTENI SANA KWA KUNISIKILIZA
   MUNGU IBARIKI TANZANIA

Comments