Disable Preloader

News

Maadhimisho ya Kumbukumbu ya Dr. Reginald Mengi kufanyika mwezi Mei

Taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa na bi. Shimimana ntuyabaliwe, mkurugenzi wa taasisi ya dr. Reginald mengi kwa watu wenye ulemavu (drmf) tarehe 23 machi 2020 kuhusu mwezi wa kujitolea kwa jamii kwa maadhimisho ya kumbukumbu ya muasisi wao dr. Reginald a. Mengi itakayojulikana kwa jina la #ubuntu

Kwa niaba ya taasisi ya Dr. Reginald Mengi Persons with Disabilities Foundation, nitoe pole kwa Mheshimiwa Rais John Pombe Magufuli pamoja na watanzania wote kwa janga la ugonjwa wa Corona (COVID19). Nichukue fursa hii kuwahamasisha watanzania wenzangu kuzingatia masharti yanayotolewa na Serikali yetu pamoja na wataalamu wa afya ili kujiepusha wewe pamoja na watanzania wenzetu.

Kwa kuzingatia maelekezo ya Serikali yetu ya kudhibiti ugonjwa huu wa Corona, tunatumia njia hii ya kutoa taarifa kwa umma wa watanzania bila ya kukutana mubashara na wanahabari. Hivyo basi nichukue fursa hii kuwaomba vyombo vyote vya habari pamoja na wanahabari kupokea taarifa hii inayohusu matayarisho ya maadhimisho ya kumbukumbu ya muasisi wetu Dr. Reginald Mengi. Maadhimisho haya yamepangwa kufanyika mwezi wa Mei 2020.

Tunaamini kuwa kwa jitihada zinazofanywa na serikali yetu kuudhibiti ugonjwa huu wa Corona, mpaka kufikia mwezi Mei, shughuli zinazohusu mikusanyiko ya watu zitakuwa zimerejea.

Ndugu wanahabari, Taasisi ya Dr. Reginald Mengi Persons with Disabilities Foundation inaandaa shughuli mbalimbali za kumbukumbu ya muasisi wetu marehemu Dr. Reginald Mengi zitakazofanyika katika mwezi wa Mei 2020.

Mwezi wa Mei ni muhimu kwetu kwasababu umebeba matukio matatu muhimu ambayo ni kumbukumbu ya mwaka mmoja tangu muasisi wetu alipofariki tarehe 2 Mei 2019, pia siku yake ya kuzaliwa ni tarehe 29 Mei na tarehe 18 Mei 2018 taasisi hii ilisajiliwa rasmi.

Ndugu wanahabari, tutaendesha kampeni ya kuwahamasisha watanzania popote pale walipo, taasisi, mashirika, na vikundi vya kijamii kuutumia mwezi wa Mei kila mwaka kufanya matendo mbalimbali ya kujitolea kwa kumbukumbu ya Dr. Reginald A. Mengi. Kampeni hii itajulikana kwa jina la #UBUNTU.

UBUNTU ni neno la kabila la wazulu kutoka Afrika ya Kusini likimaanisha “UTU” au “UTU WANGU NI BORA KUPITIA UTU WETU SOTE” au “MOYO WA KUJITOLEA KWA BINADAMU MWENZAKO”. Taasisi yetu inaamini kuwa neno hili moja UBUNTU linatosha kumtambulisha marehemu Dr. Mengi kikamilifu.

Ndugu wanahabari, Katika uhai wake Dr. Mengi alijitolea na kufanya mambo mengi katika jamii ya watanzania. Mkono wake ulikuwa mrefu na mpana na alijitoa akiwa na tabasamu la bashasha bila kuchoka. Aligusa na kuleta tofauti katika maisha ya watanzania wengi aliowafikia. Alileta matumaini kwa watanzania wenzake. Alikuwa nyota na kinara wa moyo wa kujitolea.

Tunawaomba watanzania kwa umoja wao kutuunga mkono na kuleta tabasamu kwa watanzania wenzao. Tunawasihi sana watanzania kuendeleza mshumaa wa matumaini kwa kujenga moyo wa kujitolea kwa jamii. Tukumbuke kuwa kujitolea ni moyo na sio utajiri. Hivyo basi tunawahamasisha watanzania wote kwa ujumla wao kujitolea kwa jamii inayowazunguka kupitia taasisi, mashirika, vikundi vya kijamii au watu binafsi kushiriki matukio ambayo tumeyandaa au kwa kupitia njia nyingine ambazo watapenda kuzitumia ili kujitolea kwa jamii zinazowazunguka

Ndugu wanahabari, katika kuadhimisha maisha ya Dr. Reginald Mengi, kwa mwezi Mei 2020, hususani moyo wake wa kujitolea kwa jamii, tumeandaa matukio yafuatayo;

i. Michezo Jumuishi “Tembea kwenye Viatu Vyangu “

Kwa kushirikiana na COPE pamoja na Jakaya Kikwete Youth Park, tumeandaa michezo jumuishi ambayo itashirikisha watoto wa shule za msingi wenye na wasio na ulemavu. Michezo hii itakutanisha watoto elfu moja kutoka shule za msingi za mjini Dar es Salaam. Vilevile tumeandaa “tembea kwenye viatu vyangu” michezo itakayojumuisha watu mashuhuri watakaocheza michezo maalum kwaajili ya watu wenye ulemavu. Michezo hii itawajumuisha waheshimiwa wabunge, mabalozi, wanamichezo pamoja na watu mashuhuri..

Michezo hii imelenga kutambua changamoto zinazowakabili watu wenye ulemavu, fursa mbalimbali kwa watu wenye ulemavu kupitia michezo na kuhamasisha jamii kuendeleza moyo wa kujitolea kuzikabili ili kuwezesha jamii jumuishi

Tumemuomba Mheshimiwa Mama Samia Suluhu, Makamu wa Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, kuwa Mgeni Rasmi katika michezo hii, ambayo itakuwa ya uzinduzi wa maadhimisho haya ya kumbukumbu ya Dr. Reginald A. Mengi. Michezo hii imepangwa kufanyika kufanyika tarehe 7 ya mwezi Mei, 2020 kuanzia saa mbili asubuhi hadi saa sita mchana.

ii. Changia Damu “Linda Uhai”

Kwa kuzingatia UBUNTU, kujitolea damu ili kuokoa maisha ya binadamu mwenzako ni tendo lenye alama ya utu. Kwa kushirikiana na Mpango wa Taifa wa Damu Salama pamoja na vyama vya watu wenye ulemavu tumepanga kuwahamasisha watanzania popote walipo wajitokeze kwa umoja wao kujitolea damu katika maadhimisho haya ya kumbukumbu ya Dr. Mengi. Wachangiaji wanatarajiwa kuwa watu wenye na wasio na ulemavu. Utaratibu wa kuchangia damu katika vituo mbalimbali utatangazwa.

Tumemuomba Waziri wa Afya, Jinsia na Watoto, Mheshimiwa Ummy Mwalimu kushirikiana nasi na kuzindua kampeni hii ya kuchangia damu. Uzinduzi umepangwa kufanyika tarehe 08 ya mwezi Mei mjini Dar es Salaam katika viwanja vya Mbagala Zakeem vya jijini Dar es Salaam.

iii. Panda Miti “Linda Vizazi Vijavyo”

Dr. Mengi alipanda miti ipatayo 24,000,000 katika jitihada za kulinda uoto wa asili wa mlima Kilimanjaro. Katika kumbukumbu hii ya kuenzi matendo haya ya kujitolea #UBUNTU, taasisi yetu itapanda miti kwa kushirikiana na watu wenye ulemavu katika mlima Kilimanjaro pamoja na shule kadhaa za msingi zilizoko makao makuu Dodoma pamoja na Dar es Salaam.

Vilevile tutawahamasisha watanzania popote pale walipo wapande miti ili kulinda uoto wa asili na kujikinga na athari za mabadiliko ya hali ya nchi kwa faida yetu na kwa vizazi vijavyo. Tumemuomba Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, Mheshimiwa Mussa Zungu kuwa Mgeni Rasmi siku ya tarehe 12 mwezi Mei mjini Dodoma. Vilevile, tumemuomba Waziri wa Maliasili na Utalii Mheshimiwa Dr. Hamisi Kigwangwala, kushirikiana nasi kuwa Mgeni Rasmi siku tutakapopanda miti katika Mlima Kilimanjaro tarehe 29 Mei 2020.

iv. Matembezi Jumuishi ya Hisani ya Kumbukumbu ya Dr. Reginald Mengi (Dr. Reginald Mengi Inclusive Walkathon)

Taasisi imeandaa matembezi ya hisani, yatakayojumuisha kutembea na kukimbia ambayo ni jumuishi. Matembezi haya yatajumuisha watu wenye ulemavu, vikundi vya jogging pamoja na jamii ya watanzania. Matembezi haya yatakuwa ndio kilele cha maadhimisho ya kumbukumbu ya Dr. Reginald Mengi. Baada ya matembezi washiriki pamoja na wananchi wengine watapata nafasi ya kuchangia damu.

Matembezi haya ya hisani yanafanywa kwaajili ya kuchangia ukarabati wa darasa la komputa katika shule ya Ufundi Yombo kwaajili ya Watu wenye Ulemavu pamoja na kuchangia vifaa visaidizi kwa jamii ya watu wenye ulemavu.

Matembezi haya jumuishi yatazinduliwa na kuhitimishwa katika viwanja vya Mnazi mmmoja vilivyoko katika Manispaa ya Ilala. Tumemuomba Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kushiriki matembezi haya kama Mgeni Rasmi, siku ya Jumapili tarehe 31 Mei 2020.

Ombi Maalum kwa Ndugu zetu Waandishi wa Habari,

Dr. Reginald Mengi, alikuwa ni mmoja wa waanzilishi wa vyombo vya habari binafsi hapa nchini. Alijitoa kwa hali na mali katika kujenga tasnia hii ikiwa ni pamoja na kujenga kada ya wanahabari makini na wenye weledi. Mara nyingi alijitoa kulinda ustawi wa wanahabari.

Kwa kutambua mchango muhimu na alama alizoziacha Dr. Mengi katika tasnia ya habari, tunaleta maombi maalum kwa wanahabari wote pamoja na wamiliki wa vyombo vya habari, mkiwa wadau muhimu katika kampeni hii kuhamasisha umma wa watanzania pamoja na taasisi kuupokea na kuutumia mwezi wa Mei kwa kufanya matendo ya kujitolea kusaidia jamii inazowazunguka kwa kumbukumbu ya Dr. Reginald A. Mengi. Kwa namna ya kipekee kabisa, tunawaomba waandishi wa habari kuendelea kutusaidia katika kampeni hii kuuelimisha umma kuhusu moyo mkubwa wa kujitolea wa muasisi wetu kupitia vipindi maalum, makala, na kumbukumbu za hotuba zake ili kuwahamasisha umma wa watanzania kuupokea mwezi Mei kuwa mwezi wa kujitolea katika nyanja mbalimbali hapa Tanzania. Ninawashukuru sana kwa kutupa nafasi katika vyombo vyenu vya habari.

Mungu Ibariki Tanzania, Mungu wabariki watanzania wote.

……………………………………………………………………………………………..,

Taarif fupi ya taasisi ya Dr. Reginald Mengi inayohudumia watu wenye ulemavu;

Usajili

Taasisi ya Dr. Reginald Mengi Persons with Disabilities Foundation (DRMF) ni TRUST iliyosajiliwa tarehe 18 Mei, 2018 katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya sharia namba (cap 318 0f 2002 ya Trustees Incorporation Act).

Dira

Dira yetu ni kujenga jamii jumuishi ambayo imewezeshwa ambayo watu wenye ulemavu wanapewa haki zao za msingi kwa kuzingatia upendo, utu na heshima.

Dhima

Dhima ya taasisi yetu ni kuwapa heshima, kuwapa hamasa na kuwawezesha watu wenye ulemavu.

Comments