Disable Preloader

News

Kampeni ya ubuntu kupokea misaada kwaajili ya wahitaji

Taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa na Bi. Shimimana Ntuyabaliwe, Mkurugenzi wa taasisi ya Dr Reginald Mengi kwa watu wenye ulemavu (DRMF) Tarehe 15 mei 2020 Kuhusu mwezi wa kujitolea kwa jamii kwa maadhimisho ya Kumbukizi ya muasisi wao Dr. Reginald A. Mengi Itakayojulikana kwa jina la

Kwa niaba ya wadhamini wa taasisi ya Dr. Reginald Mengi Persons with Disabilities Foundation, nitoe pole kwa Mheshimiwa Rais John Pombe Magufuli pamoja na watanzania wote kwa janga la ugonjwa wa Corona (COVID19). Nichukue fursa hii kuwahamasisha watanzania wenzangu kuzingatia masharti yanayotolewa na Serikali yetu pamoja na wataalamu wa afya ili kujiepusha wewe pamoja na watanzania wenzetu.

Kwa kuzingatia maelekezo ya Serikali yetu ya kudhibiti ugonjwa huu wa Corona, tunatumia njia hii ya kutoa taarifa kwa umma wa watanzania bila ya kukutana mubashara na wanahabari. Hivyo basi nichukue fursa hii kuwaomba vyombo vyote vya habari pamoja na wanahabari kupokea taarifa hii inayohusu matayarisho ya maadhimisho ya kumbukumbu ya muasisi wetu Dr. Reginald Mengi. Maadhimisho ambayo yalipangwa kufanyika mwezi wa Mei 2020.

Kutokana na maelekezo ya Serikali kuhusu hatua maalum na jitihada za kuudhibiti ugonjwa huu wa Corona, ni wazi kuwa mwezi Mei, shughuli zinazohusu mikusanyiko ya watu bado hazijarejea.

Ndugu wanahabari, Taasisi ya Dr. Reginald Mengi Persons with Disabilities Foundation inatangaza rasmi kusimamisha kwa muda shughuli za maadhimisho ya muasisi wetu Dr. Reginald Mengi ambazo zinahusisha mikusanyiko ya watu hadi hapo zitakapotangazwa tena. Shughuli ambazo tumeziahiirisha ni “Michezo Jumuishi ya Tembea kwenye Viatu Vyangu”, “Matembezi Jumuishi ya Hisani ya Dr. Reginald Mengi” pamoja na kampeni ya “Panda Miti, Linda Vizazi Vijavyo”.

Ndugu wanahabari, ninayo furaha kusema kuwa, Taasisi yetu imeamua kutumia kampeni hii ya UBUNTU ili kuunga mkono Serikali yetu, wananchi pamoja na wadau mbalimbali kupambana na janga hili la ugonjwa wa CORONA.

Ndugu wanahabari, tutaendesha kampeni ya kuwahamasisha watanzania popote pale walipo, taasisi, mashirika, na vikundi vya kijamii kuutumia mwezi wa Mei, kusaidia jamii zinazowazunguka hususani wale ambao wanauhutaji.

Ndugu wanahabari, Taasisi yetu kwa kushirikiana na Mpango wa Taifa wa Damu Salama pamoja na Rotary Club ya Mikocheni pamoja, tutaendesha kampeni ya kuwahamasisha watanzania wenzetu popote walipo kwa nafasi zao, pamoja na taasisi mbalimbali kuupokea mwezi wa Mei na kujitolea kwa jamii zenye mahitaji.

Ndugu wanahabari, kampeni hii inahamasisha kuwasaidia makundi ambayo yana uhitaji ikiwa ni pamoja na watu wenye ulemavu, wazee ambao wanatunzwa katika nyumba maalum pamoja na watoto wanaolelewa katika vituo.

Ndugu wanahabari, kampeni hii itahamasisha uchangiaji wa Barakoa, Sabuni, Vitakasa Mikono pamoja na Futari. Ndugu wanahabari, vilevile kampeni hii itahamasisha uchangiaji wa damu. Mahitaji ya damu kama tiba bado yako palepale, hususani kwa wakina mama wajawazito ambao wanajifungua pamoja na wahanga wa ajali.

Ndugu wanahabari, kwakuwa kumbukizi hii ya moyo wa kujitolea wa Dr. Reginald Mengi inafanyika mwezi wa Mei, tunapata faraja sana kuwa kampeni hii inafanyika katika kipindi cha Mwezi wa toba na sadaka, mwezi mtukufu wa mfungo wa Ramadhani.

Ndugu wanahabari, basi nichukue fursa hii kuwaalika ndugu zetu watanzania kutuunga mkono na kujitolea kwa hali na mali ili makundi haya yaweze kupata msaada ambao wanauhitaji sana.

Ndugu wanahabari, nichukue fursa hii kumshukuru sana mke wa muasisi wetu na mdhamini wa taasisi yetu, Mama Jacqueline Mengi, kwa kuonyesha njia na kuchangia barakoa kwa watoto wenye ulemavu pamoja na wazee. Vilevile amejitolea chakula ili familia za watu wenye ulemavu ziweze kupata futari katika mwezi huu wa mfungo mtukufu wa Ramadhani.

Ndugu wanahabari, vilevile nitoa shukrani za kipekee kabisa kwa taasisi ya Hindu Swayam Sevak San (HSS) kutoka kwa wenzetu jamii ya wahindu ambao siku ya leo wamekuja kutuunga mkono na kujitolea vitu mbalimbali ikiwemo vitakasa mikono, barakoa, sabuni pamoja na gloves.

Ndugu wanahabari, tunafurahi kuwa siku ya leo tumekabidhi vifaa mbalimbali kwa walengwa kama ifuatavyo

  • Shirikisho la Vyama vya Watu Wenye Ulemavu, likiwakilishwa na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wakina Mama na Watoto, Mheshimiwa Diwani Bi. Nuru Awadhi pamoja na Katibu mkuu wa Jumuiya hiyo Bi. Blandina Sembu. Shirikisho limepokea Barakoa pamoja na Futari kwaajili ya familia za watu wenye ulemavu.
  • Mpango wa Taifa wa Damu Salama, ukiwakilishwa na Mkuu wa Kitengo Cha Ukusanyaji Damu Kanda ya Mashariki Bi. Judith Chale ambae aliambatana na Bi. Fatuma Mujungu, Afisa Uhusiano wa Kanda ya Mashariki, walipokea barakoa, vitakasa mikono, sabuni pamoja na gloves. Vifaa hivi vitatumika kwa wachangiaji damu kwa hiari.

Ndugu wanahabari, napenda kuwakumbusha tena kuwa UBUNTU ni neno la kabila la wazulu kutoka Afrika ya Kusini likimaanisha “UTU” au “UTU WANGU NI BORA KUPITIA UTU WETU SOTE” au “MOYO WA KUJITOLEA KWA BINADAMU MWENZAKO”. Taasisi yetu inaamini kuwa neno hili moja UBUNTU linatosha kumtambulisha marehemu Dr. Mengi kikamilifu.

Ndugu wanahabari, Katika uhai wake Dr. Mengi alijitolea na kufanya mambo mengi katika jamii ya watanzania. Mkono wake ulikuwa mrefu na mpana na alijitoa akiwa na tabasamu la bashasha bila kuchoka. Aligusa na kuleta tofauti katika maisha ya watanzania wengi aliowafikia. Alileta matumaini kwa watanzania wenzake. Alikuwa nyota na kinara wa moyo wa kujitolea.

Tunawaomba watanzania kwa umoja wao kutuunga mkono na kuleta tabasamu kwa watanzania wenzao. Tunawasihi sana watanzania kuendeleza mshumaa wa matumaini kwa kujenga moyo wa kujitolea kwa jamii. Tukumbuke kuwa kujitolea ni moyo na sio utajiri. Hivyo basi tunawahamasisha watanzania wote kwa ujumla wao kujitolea kwa jamii inayowazunguka kupitia taasisi, mashirika, vikundi vya kijamii au watu binafsi kujitolea kwa jamii zinazowazunguka

Changia Jamii yenye Mahitaji
Janga la Corona limeleta madhara makubwa katika dunia. Jamii za watu ambao wanaishi katika mazingira ambayo sio rafiki huathirika zaidi. Taasisi yetu kwa kushirikiana na Rotary Club ya Dar es Salaam Mikocheni tumeainisha jamii hizo kuwa ni watu wenye ulemavu, wazee wanaotunzwa katika vituo maalum pamoja na watoto wanaolelewa katika vituo.
Ili kusaidia jamii hizi kukabiliana na athari za janga hili tumeainisha baadhi ya mahitaji ambayo yanahitajika kwa sasa kuwa ni barakoa, sabuni, vitakasa mikono pamoja na chakula. Michango ya mali itapokelewa katika ofisi zetu zilizopo Mikocheni Kwa Warioba, Kitalu namba 164C, katika barabara ya Mwai Kibaki. Vilevile tunapokea michango ya pesa kwenda kwenye akaunti yetu iliyopo katika benki ya CRDB
Jina la Akaunti: Dr. Reginald Mengi PWD Foundation
Tawi: Mikocheni
Benki: CRDB Bank
Namba ya Akaunti: 0150391480200
Wasiliana nasi kwa maelezo zaidi kupitia namba 0736 280 491 au 0766 815 088.

Changia Damu “Linda Uhai”
Kwa kuzingatia UBUNTU, kujitolea damu ili kuokoa maisha ya binadamu mwenzako ni tendo lenye alama ya utu. Kwa kushirikiana na Mpango wa Taifa wa Damu Salama pamoja na vyama vya watu wenye ulemavu tumepanga kuwahamasisha watanzania popote walipo wajitokeze kwa umoja wao kujitolea damu katika maadhimisho haya ya kumbukumbu ya Dr. Mengi.
Wachangiaji mmoja mmoja atembelee ofisi za Kitaifa na kanda ambazo ni (Ilala Mchikichini kwa Dar es Salaam, Hospitali ya Bugando Mwanza, Hospitali ya Kitete Tabora, Hospitali ya Ligula Mtwara, Hospitali ya KCMC Moshi, Hospitali ya Meta Mbeya, na Hospitali Kuu Dodoma) au hospitali za Mkoa popote ulipo.

Ndugu wanahabari, wataalamu wa afya wanaweza kukufuata huko uliko iwapo

  • wewe pamoja na majirani zako mtapenda kuchangia damu au
  • Wafanyakazi wa ofisi au viwanda wangependa kuchangia damu, Piga simu hizi za ofisi za Mpango wa Damu Salama Makao Makuu ili kupata maelekezo ya ziada (+255 739 613 000 au +255 656 262 311) Unaweza kuwasiliana na ofisi za kanda (Mwanza – 0735 553 727; Tabora – 0734 120 900; Mtwara – 0737 966 664; Moshi – 0678 093 091; Mbeya – 0743 711 492; Dodoma – 0658 535 433)
  • Shukrani Maalum kwa Ndugu zetu wa vyombo vya Habari,
    Kwa niaba ya wadhamini wa taasisi yetu ya Dr. Reginald Mengi, PWD Foundation, nichukue fursa hii kuwashukuru sana wale wote ambao wamekuwa wakiandika makala na kutoa taarifa kwa UMMA wakiwakumbusha na kuwaelemisha watanzania kuhusu mambo mbalimbali ambayo aliyafanya Dr. Reginald Mengi.
    Kwa kutambua mchango muhimu na alama alizoziacha Dr. Mengi katika tasnia ya habari, tunaendelea kuleta maombi maalum kwa wanahabari wote pamoja na wamiliki wa vyombo vya habari, mkiwa wadau muhimu katika kampeni hii kuhamasisha umma wa watanzania pamoja na taasisi kuupokea na kuutumia mwezi wa Mei kwa kufanya matendo ya kujitolea kusaidia jamii inazowazunguka kwa kumbukumbu ya Dr. Reginald A. Mengi.
    Kwa namna ya kipekee kabisa, tunawaomba waandishi wa habari kuendelea kutusaidia katika kampeni hii kuuelimisha umma kuhusu moyo mkubwa wa kujitolea wa muasisi wetu kupitia vipindi maalum, makala, na kumbukumbu za hotuba zake ili kuwahamasisha umma wa watanzania kuupokea mwezi Mei kuwa mwezi wa kujitolea katika nyanja mbalimbali hapa Tanzania. Ninawashukuru sana kwa kutupa nafasi katika vyombo vyenu vya habari.

    Mungu Ibariki Tanzania, Mungu wabariki watanzania wote.

    Taarif fupi ya taasisi ya Dr. Reginald Mengi inayohudumia watu wenye ulemavu;
    Usajili
    Taasisi ya Dr. Reginald Mengi Persons with Disabilities Foundation (DRMF) ni TRUST iliyosajiliwa tarehe 18 Mei, 2018 katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya sharia namba (cap 318 0f 2002 ya Trustees Incorporation Act).

    Dira
    Dira yetu ni kujenga jamii jumuishi ambayo imewezeshwa ambayo watu wenye ulemavu wanapewa haki zao za msingi kwa kuzingatia upendo, utu na heshima.

    Dhima
    Dhima ya taasisi yetu ni kuwapa heshima, kuwapa hamasa na kuwawezesha watu wenye ulemavu.

Comments